|
282. Enyi mlio amini! Mnapo kopeshana deni kwa
muda ulio wekwa, basi andikeni. Na mwandishi aandike baina yenu kwa uadilifu,
wala mwandishi asikatae kuandika. Aandike kama alivyo mfunza Mwenyezi Mungu.
Na mwenye deni juu yake aandikishe; naye amche Mwenyezi Mungu, Mola wake
Mlezi. Wala asipunguze chochote ndani yake. Na akiwa mwenye kudaiwa ni
mtu aliye pumbaa au mnyonge au hawezi kuandikisha mwenyewe, basi aandikishe
mlinzi wake kwa uadilifu. Na mshuhudishe mashahidi wawili katika wanaume
wenu. Ikiwa hapana wanaume wawili, basi mwanamume mmoja na wanawake wawili
katika mnao waridhia kuwa mashahidi. Ili ikiwa mmoja wao akipotea, mmoja
wao amkumbushe mwengine. Na mashahidi wasikatae waitwapo. Wala msipuuze
kuliandika deni likiwa dogo au kubwa mpaka muda wake. Hayo ndiyo haki zaidi
mbele ya Mwenyezi Mungu, na ndiyo sawa zaidi kwa ushahidi, na vyema zaidi
ili msiwe na shaka. Ila ikiwa ni biashara ya mkono-kwa-mkono baina yenu,
basi hapo si vibaya kwenu msipo iandika. Lakini mnapo uziana wekeni mashahidi.
Wala asitiwe matatani mwandishi wala shahidi. Na mkifanya hivyo basi hakika
hilo ni kosa kwenu. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi
wa kila kitu.
|