187. Mmehalalishiwa usiku wa Saumu kuingiliana
na wake zenu. Wao ni vazi kwenu, na nyinyi ni vazi kwao. Mwenyezi Mungu
anajua kwamba mlikuwa mkizikhini nafsi zenu. Kwa hivyo amekukubalieni toba
yenu na amekusameheni. Basi sasa changanyikeni nao na takeni aliyo kuandikieni
Mwenyezi Mungu. Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri
katika weusi wa usiku. Kisha timizeni Saumu mpaka usiku. Wala msichanganyike
nao, na hali mnakaa Itikafu msikitini. Hiyo ni mipaka ya Mwenyezi Mungu,
basi msiikaribie. Namna hivi Mwenyezi Mungu anabainisha Ishara zake kwa
watu ili wapate kumcha.
|